HISTORIA FUPI YA SHULE |
Shule ilianzishwa rasmi mwaka 1979 ikijulikana kwa jina la HUDUMA JWTZ CENTRE na kimsingi ilianza ikiwa ni kituo cha kufanyia mtihani. Shule ilianzishwa kwa lengo la kuwaendeleza Wanajeshi ambao hawakuwa wamefikia kidato cha nne kwa wakati huo. Shule ilianzia ilipo shule ya Msingi Huduma kabla ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwl. Julius Kambarage Nyerere kuamuru majengo hayo yatumike kufundishia watoto wadogo yaani, shule ya msingi na shule ya sekondari itafutiwe eneo lingine Hapo ndipo uongozi wa 411 KJ kwa wakati huo ulipotekeleza agizo hilo na kuanzisha majengo ya sekondari katika eneo hilo. Shule ilianza kwa majengo ya bati toka chini hadi juu. Baada ya lengo la JWTZ la kusomesha Wanajeshi wote angalau kufikia kidato cha nne kufanikiwa kwa asilimia kubwa na kufutwa rasmi kwa mpango huo, uongozi wa JWTZ uliona ni busara kuendelea na shule hizo za sekondari kwa lengo la kutoa huduma ya elimu kwa familia za Wanajeshi na kwa raia. Shule hii ilisajiliwa rasmi na Wizara ya Elimu na utamaduni mwaka 1995 kama shule nyingine binafsi za sekondari na kubadilishwa jina kutoka HUDUMA JWTZ CENTRE kituo kilichokuwa na Usajili wa Baraza la Mitihani wa P0336 na kuitwa Shule ya Sekondari Ruhuwiko. Mabadiliko hayo yalipelekea kupewa namba mpya ya usajili S0576 na pia usajili wa Baraza la Mitihani la Tanzania kwa namba S0751. Shule ilisajiliwa kwa udhamini wa Nyumbu Project - Kibaha kwa kuzingatia taratibu za Wizara ya Elimu na Utamaduni kwa wakati huo. |